Fortunatus Buyobe Profile picture
Pool of thoughts. A commander of the hand to mouth battalion. Environmental Pioneer. Social Engineer. #CertifiedMchapaUzi . Telegram: https://t.co/aEEOOryJWO

Jan 8, 2022, 18 tweets

Hii ilikuwa ni miaka ya '90 mwanzoni, tukitokea pembezoni mwa mgodi wa Mwadui, tulifahamika kwa jina la "Wabeshi".

Zana zetu za kazi ilikuwa ni sululu, chepe na majembe yaliyonolewa sana, tulikabiliana na jeshi la polisi la mgodi wa Mwadui waliokuwa na kikosi cha farasi na mbwa wenye uweredi mkubwa sana na mafunzo ya hali ya juu.

Nakumbuka siku rafiki zangu wawili walivyouwawa kwa kuumwa na mbwa sehemu za siri na jirani yangu Jilingumika Masufulia alivyopigwa risasi ya kichwa akivuka fensi ya mgodi wa Mwadui.

Almasi tuliibatiza jina la "ng'ana", na ilikuwa hauwezi kwenda kuiba bila kuchanjwa chale za kwapani na matakoni. Mganga wetu mkubwa alikuwa ni Mzee maarufu sana wa Kijiji cha MWIGUMBI, Nje kidogo ya mgodi, huyu ndio mzee aliyetupa dawa na kinga wakati wa kwenda kuiba almasi,

Nilikuwa na miaka 16 nimemaliza darasa la saba shule ya msingi Luhumbo.Tajiri wetu mkubwa alikuwa mwarabu wa Maganzo maarufu kwa jina la Abeid,huyu alitupikia vitumbua na chai kabla ya kwenda mgodini kuiba almasi, na chote tulichokipata tulipeleka kwake kama tajili na kulipa

Tajiri Abeid hakuwa mtu "rahisi rahisi", yeye mganga wake alikuwa anatokea kijiji cha Idukilo, mganga hatari sana aliyekuwa na madawa ya kisukuma ambayo yaliwabadilisha watu na kuwa mbwa mwitu au nyani pindi walipoingia ndani ya mgodi kuiba,

tajiri Abeid alikuwa anaishi kijiji cha Maganzo, akiwa na duka la bidhaa la kuzugia,lakini deal zake kubwa ilikuwa ni kununua almasi na kuziuza kwa matajili wakubwa wa Mwanza na Shinyanga mjini.

Almasi zote tulizopeleka kwa Abaeid zilikuwa zinatunzwa na mbuzi dume, beberu mkubwa aliyekuwa anazimeza na kuzihifadhi tumboni hadi mteja atakapokuja,hata polisi wakifika na ku-search vipi,wasiongeziona almasi kwani beberu alikuwanazo tumboni,

hakuwa beberu wa kawaida maana alikuwa na chumba chake na alilala ktk godoro. Mbuzi hakula nyasi wala majani ya miti, bali vitumbua, chai na "maparage". Kipindi hicho hatukuwa na ruhusa ya kuongea juu ya mbuzi yule, tulimuogopa na kumtii zaidi hata ya kiongozi wetu.

Tajiri wa uhakika alikuwa Fantomu wa maeneo ya Mipa,huyu hakuonana na sisi wabeshi maana tulikuwa watu "wadogo" sana, bali alipitia kwa Abeid na waarabu wengine wa Maganzo.

Maisha ya kuwa "mbeshi" yalikuwa magumu sana,maana kifo na kujeruhiwa ilikuwa ni njenje,tuliuwa na kuuwawa.

Polisi, mbwa na farasi waliokuja bila tahadhari waliuwawa kwa chepe zilizonolewa na mapanga. Tukio moja nalokumbuka ni la mwenzetu Masunga kumuua mbwa wa polisi kwa kumkata na chepe mdomoni na kuutenganisha mdomo pande mbili.

Wenzetu wengi walikufa tukiwa bwawani tukiiba,wengi walizama kwenye tope liliotokana na mabaki ya kusafishwa kwa almasi ambayo sisi tulikuwa tunakwenda kuchota na kuchekecha upya,

bwawa hili la tope zito lilukuwa karibu na "sorting area" ambayo ililindwa kwa kiasi kikubwa sana. Lakini kwa imani ya chale za mganga wa MWIGUMBI na Idukilo watu wengi tulikuwa na ujasiri wa kukatiza kila mahali bila hofu.

Wengi waliojeruhiwa na kuumizwa walilazwa ktk hospitali ya Mwadui.Siku nilipoamua kuacha "kazi" hii na kurudi shule,ilikuwa ni siku hatari sana... binamu yangu kipenzi Luhende alipigwa risasi ya kichwa na ubongo kutawanyika, mbele ya macho yangu Luhende alikufa bila kuomba maji.

Askari wakiwa umbali wa kama mita 100,sisi tukiwa na makarai yetu na chekecheke tukiambaaambaa pembeni ya reli maeneo ya SONGWA ktk njia ya mzunguko kuelekea Maganzo tuliwekwa katikati yao na kuuliwa baadhi yetu.

Katika kundi la wabeshi kumi, saba walikufa hapo hapo..watatu walifia hospitali na mimi pekee nilipona baada ya kujitumbukiza kwenye bwawa la maji ya kunywea mifugo, niliogolea chinichini kwa chini na kuibukia upande wa matete, ambapo nilikaa ndani ya maji zaidi ya masaa 12

Tuendelee na wahabeshi?

Share this Scrolly Tale with your friends.

A Scrolly Tale is a new way to read Twitter threads with a more visually immersive experience.
Discover more beautiful Scrolly Tales like this.

Keep scrolling