Baada ya kitambo chote nakiri kuwa, kama kukutana kwetu ni ajari basi wewe ndiye kilema changu cha kudumu. Taswira yako haijawahi kufutika akilini mwangu. Kila wakati, kila mahali na kwa kila jambo umekuwa msukumo wangu wa ndani.
....Pupa ya kuyaendea yenye manufaa imekua si kwangu tena, bali ni kwetu, Nimepata uthubudu mara dufu ya ule niliokua nao awali. Mguso wako wa kimwili, kihisia na kinafsi unanipa nguvu ya kusogea ukiwa pamoja nami. Kwa mara nyingine naomba nikiri hilo.
Niliomba furaha na Mungu kwa mapenzi yake akanipa wewe. Siwezi kukulinganisha na dunia na nilivyomo kwasababu wewe ndiye dunia yangu. Umekusanya vingi ndani yako vinavyostawisha maisha yangu. Jukumu langu ni kukupenda na mategemeo yangu ni wewe kuupokea upendo wangu.
.....Uukamate na ufumbate, usiuache ukapeperuka. Kunirudishia upendo hiyo ni hisani yako kwangu. Itakua ni zawadi adhimu ya ziada iwapo utafanya hivyo.
Na nataka ujue kuwa, najali sana kuhusu furaha yako. Na ikiwa mimi ni sehemu ya furaha hiyo basi nitajijali pia. Ikiwa hivyo nikuhakikishie kuwa furaha yako itadumu. Nitailinda na kuiepusha juu hatari zote hata hatari hiyo ikiwa ni mimi mwenyewe.
Nipewe kalamu na wino mithili ya maji ya bahari, sitomaliza kuulezea upendo wangu kwako. Mimi si mjuzi wa lugha nyingi. Lakini lugha inayozungumzwa na moyo wangu juu ya upendo wangu kwako bado sijaipatia maneno yanayojitosheleza kuulezea.
Mungu akulinde na akutunze kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili yetu sisi vipenzi vyako.
NAKUPENDA.
Imekua kitambo kidogo. Natumai ujumbe huu utakukuta ukiwa mzima wa afya. Nimekua nikikuombea hivyo siku zote, pasi kujali ni nyakati za aina gani tumekua tukizipitia. Na hii ni kwa sababu naguswa na uwepo wako...
... Nazifurahia nyakati zako nzuri na kuogopeshwa na nyakati ambazo huwa ni mbaya kwako. Zinaogogya zaidi kwangu kwa sababu huwa zinaniathiri pia. Na hii yote ni kwasababu ninakujali.
Nakumbuka siku ya kwanza tunakutana. Nilishindwa kukuzuia, ila nilitamani usiondoke. Nuru ya uso wako iliangaza mboni za macho yangu. Kila sekunde na dakika tulizokaa pamoja zilikua ni za thamani kwangu.